JINSI YA KUJIWEKEA MALENGO KWENYE MAISHA YAKO.

 

JINSI YA KUJIWEKEA MALENGO KWENYE MAISHA YAKO.



MALENGO:

                Ni mipango au dhima au matamanio ya mtu aliyonayo juu kupata matokeo Fulani, malengo yanapozungumziwa mara nyingi hulenga kuangalia ndoto za mtu au shauku aliyonayo mtu. Na malengo hapa tunazungumzia malengo katika uchumi, malengo ambayo yanaweza kukusaidia kuwa mwongozo wa wewe kuelekea mafanikio yako ya kiuchumi, kwasababu malengo ni njia kuelekea mafanikio.

Mafanikio:

                Mafanikio ni hatua mtu anayopiga kutoka katika hali ya chini hadi hali ya juu ambapo tunaweza kusema mafanikio ni sawa na maendeleo. Mafanikio hayaji yaji tu, hapana, mafanikio yanatengenezwa hatua mpaka hatua na katika hatua kuelekea mfanikio basi lazima uzifuate, huwezi kufikia mafanikio kama hufuati hatua zinazokuongoza hadi kuyafikia mafanikio yako

Jifunze hatua kuelekea za mafanikio

Katika kelekea mafanikio lazima ukubali kujitoa kwa nguvu katika kuandaa malengo ambayo pia yananguvu na yanafuata kanuni za kuweka malengo.

Malengo Mazuri na yanayotambulika huwa yanafuata kanunu, na zifuatazo ni kanuni na sifa za malengo

KANUNI / SIFA ZA MALENGO (SMART PLANS)

Malengo kwa kawaida yanatakiwa kuwa na sifa zisizopungua tano ambazo ni

1.       Malengo yawe Maalum (SPECIFIC)

2.       Malengo yaweze Kupimika (MEASURABLE)

3.       Malengo yawe Yanafikika (ATTAINABLE)

4.       Malengo yawe Halisi (REAL)

5.       Malengo yawe na muda unaoeleweka (Time Frame)

UFAFANUZI WA KANUNI

1.       MALENGO YAWE MAALUM (SPECIFIC)

Malengo maalum ni malengo ambayo yanaeleweka na yanatambulika vizuri (Clear and identified), ni malengo ambayo hata wewe uliye yaandika utayaelewa kwamba yanataka nini, ukiwa unaandaa malengo hakisha unazingatia swala la kuelweka kwa malengo yako, Malengo smart ni malengo ambayo lazima yawe wazi na kutambulika, usiandike malengo kwa mafumbo ili mwingine asielewe la hasha unapoandika kitu kwa mafumbo umejipa kazi hata wewe kutafuta maana ya mafumbo hayo. Malengo mazuri ni yale yaliyo wazi na kueleweka, yaani wewe mwenyewe unayaelewa vizuri.

Kutengeneza malengo wazi yanahitaji pia utuvu wa namna ya kuandika, malengo wazi ni sawa na uandishi kwa kichwa cha habari au kichwa kidogo cha habari (Title/subtitle)

Mfano: kama unataka gari andika Gari RAV4 au Kununua gari RAV4

                Sio kuandika maelezo, yani mwaka huu nataka nikifanikiwa tu nipate pesa ili nione namna ya kununua gari tena RAV4 hii ni unyama sana.

Hii sio lengo, hii ni vurugu ya lengo, kwahiyo lengo liandikwe vizuri na lieleweke vyema.

2.       MALENGO YAWEZE KUPIMIKA (MEASURABLE)

Ni kweli kabisa malengo mazuri ni yale yanayopimika, yanayoweza kupimwa yaani kuchunguzika katika mzani kwamba linawezekana au haliwezekani. Lengo likiwa linapimika maana yake linaweza kuingia kwenye kuchakatwa na kuonekana namna gani linaweza kutimizwa, lakini pia lengo likiwa lenye kupimika maana yake unaweza kulilinganisha lengo hilo na malengo mengine hii itakusaidia kufanya maamuzi ya lengo gani la kutembea nalo, au kuanza nalo na kuyaweka malengo yako yote katika mpangilio.

Kiufupi, malengo kupimika maana yake ni kupima uzito wa lengo hususani kwenye matokeo yake baada ya kufanikiwa, pia umuhimu wake na namna inavyogharimu ili kulifikia, kwahiyo lengo zuri linapimika.



3.       MALENGO YAWE YANAFIKIKA (ATTAINABLE)

Ndio, malengo yanatakiwa kuwa na uwezekano, yani yawezekane kutimia au kufikiwa, ukipanga malengo ambayo huwezi kuyafikia maana yake ni kwamba hauna kazi unayoifanya isipokuwa unapoteza muda tu, malengo mazuri ni yale yanayofikika na mtu anaweza kuyatimiza.

Malengo yasiyofikika ni malengo ambayo yanamuda mrefu sana Zaidi ya umri na vyanzo vya kipato

Mfano: Unafanya biashara ya kuuza nyanya na unaweka malengo ya kusema utanunua ndege. Je, kweli utafikia lengo hili? Jibu ni hapana sio rahisi kulifikia kwa maana hiyo umeweka lengo ambalo halifikiki

HESABU NDOGO

Nyanya mtaji ni Tsh. 200,000/=

Faida kwa mwezi ni Tsh. 200,000/=

Kwa mwaka = 200,000 x 12 = 2,400,000/= hapa hujatumia kwa matumizi yoyote

Ndege inathamani mfano wa Tsh. billioni 1 = 1,000,000,000/=

Hii utaitimiza kwa muda miaka mingapi 1,000,000,000 ÷ 2,400,000 = 416.67 yaani kutimiza bilioni moja unahitaji miaka 416.67 ili uweze kununua ndege. Kwa lugha rahisi ni kwamba Malengo yako ni batili yasiyofikika. Hapa nadhani nimeeleweka vizuri.

Malengo yawe yanayofikika na hapa utaweza kufanikiwa sana.

4.       MALENGO YAWE HALISI (REAL)

Malengo yawe halisi. rafiki, ukipanga malengo yasiyo na uhalisia ni sawa na kupoteza muda, malengo yanatakiwa yawe halisi bana, yanayoonekana na kuwezekana, kwasababu malengo halisi yanayonjia halisi pia ya kuyaendea, usweke malengo kama “Kuumba mtu, Kutengeneza ndege, kutawala Dunia.” Hapa utakuwa unapoteza muda yani hauna kazi ya kufanya, swala la malengo lazima yawe halisi kuendana na mazingira, kipato na waliasili zinazokuzunguka, ili kuweka malengo halisi lazima uzingatia vile vilivyopo vinavyopatikana na kuwezekana kisha weka malengo yako.

5.       MALENGO YAWE NA MUDA UNAOELEWEKA (TIMEFRAME)

Malengo bila muda maalumu ni sawa na kutembea safari usiyoelewa unafika lini. Safari usiyoielewa inaisha lini ni bora tu kutokuifanya, maana inawezekana ikawa safari ya miaka 100 na ukajikuta unapoteza maisha na safari bado hujaimaliza. Unapoweka malengo hakikisha unayawekea na muda, usipoyawekea muda hayana maana kuwepo, hii ndio maana halisi ya mkataba. Malengo ni kama mkataba una muda maalum, mkataba usio na muda maana yake hauna mwisho, sasa ukiweka lengo la hivi sio lako hilo achana nalo. Unapotaka kuweka lengo hakikisha unaliwekea muda maalum baada ya kujua kwamba linafikika basi liwekee muda utalifikia lini. Lengo zuri linaongozwa na muda uliowekwa kuelekea lengo hilo.

HITIMISHO

Malengo mazuri yanatimia, na hata kama utakutana na changamoto nyingi lakini yanatimia, jambo la msingi ni kuhakikisha hutoi mwanya wa mtu yeyote kuzimisha malengo yako uliyojiwekea na hapa utaweza kufikia kile ambacho unatarajia kufikia kwa wakati husika. Najua unajua kwamba malengo ni mafanikio, mafanikio ni malengo, hakuna mtu yeyote aliyefanikiwa pasipo malengo.

Kwahiyo Weka malengo smart kwa kuhakikisha kuwa malengo yako yanaeleweka, yanaweza kupimika/ kulinganishwa vizuri na kuchakatwa, malengo yako yanaweza kufikiwa, malengo yako ni halisi na yenye muda maalumu wa utimilizwaji. Ukifanikiwa hapa lazima utatembea vizuri kwenye safari ya mafanikio.

Ahsante sana kwa kujifunza. Kama utakua na swali la aina yoyote basi unawezaa kuuliza hapo chini na nitakurudia ili kukupatia majibu kwa wakati, ahsante na endelea kutufuatilia.

 Imeandikwa na

                        Thobias Cosmas au Caza Von Th.

About TECHNO ONLINE RICHES

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

1 comments: